Help Children
Love them
Saidia Watoto

Friday, August 30, 2013

Diamond afundisha kivitendo suala la upendo na heshima

Watu wengi walihudhuria uzinduzi huo


Akampatia funguo zake


Tukaenda kwenye gari

Hata wapishi walimpongeza




MSANII wa muziki wa kizazi kipya Nasib Abdul, Diamond  juzi alimkabidhi gari mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini aliyestaafu muziki hivi karibuni Muhidin Gurumo.

Diamond alimkabidhi mzee huyo gari hilo wakati wa hafla ya kuzindua video ya wimbo wake mpya uitwao My Number One.

Blog hii limelichukulia tukio hilo kuwa ni kama elimu ambayo Diamond ameamua kuitoa kwa watu hasa jamii ya wanamuziki wenzake ya kuheshimu na kuendeleza maisha ya wengine.


Mzee Gurumo ametumikia bendi nyingi ambazo hazijawahi hata kumsaidia mabati ya kujengea nyumba lakini kwa Diamond ameonesha zaidi ya mfano kwa mzee huyo 
Diamond baada ya kuzungumzia video yake hiyo hususan katika suala la gharama na changamoto aliyokutana nazo wakati wa kutengeneza video hiyo na ndipo alipomuita stejini mzee Gurumo.

Diamond alianza kwa kusema namna ambavyo amekuwa akimpenda na kumheshimu mzee Gurumo na kisha akaendelea kusisitiza kuwa amesikitishwa na namna mzee huyo anavyohangaika kwa sasa.

Alimuita stejini na kisha akamkabidhi funguo wa gari hali iliyopelekea wageni waalikwa kupiga kelele za kushangilia baada ya kuguswa na tukio hilo.

Bada ya hapo Diamond alimshika mkono mzee huyo na kisha wakiongozana na wageni waalikwa kwa pamoja walitoka nje na kwenda kuliangalia gari hilo.

Baada ya hapo wageni hao pamoja na Diamond walirudi tena ndani na kuendelea na ratiba kama kawaida.

Awali akizungumzia Video yake hiyo alisem akuwa imemgharimu zaidi ya milioni 50 ambapo aliitengenezea nchini Afrika Kusini.

Ni Video nzuri na ya aina yake ambayo imegusa mazingira halisi ya maisha ambayo alikuwa akiyaimba katika wimbo wake huo wa mapenzi.
Mwisho

Thursday, August 22, 2013

Wanafunzi elimu ya juu waonywa dhidi ya siasa






Na Mwandishi Wetu

WANAFUNZI wa vyuo vya elimu ya juu nchini wameonywa dhidi ya kuteua au kuchagua wajumbe wa kisiasa kugombea uongozi nchini.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Donati Salla, ilisema hilo ni jukumu la vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na vinavyotambulika.

“Shughuli za serikali za wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu ni masuala ya wanafunzi na ubora wa taaluma itolewayo katika chuo husika na mengine ya kitaifa, lakini si kwa ushabiki wa kisiasa au kutetea kundi au maslahi ya watu fulani,” ilisema taarifa hiyo.

Ilisema vikao vyote vinavyohusu mjumuiko wa serikali za wanafunzi, vinapaswa kuitishwa na kuratibiwa na Tahliso na si taasisi nyingine yoyote.

Taarifa hiyo ilitolewa kutokana na mkutano wa baadhi ya viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini uliofanyika Morogoro, ukikutanisha baadhi ya viongozi waandamizi wa wanafunzi ukiandaliwa  na Taasisi ya Kupambana na Maadui Ujinga, Maradhi na Umaskini (FPID).

Mkutano huo ulijadili masuala ya utofauti wa kipato kwa Watanzania, ubora wa elimu hasa vijijini na fursa za ajira.

“Lakini kubwa lililoibuka katika mkutano huu na kuchukua uzito mkubwa ni suala la nani awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015,” ilisema taarifa na kuongeza kuwa Tahliso ilisikitishwa na kulaani matukio yaliyojitokeza katika mkutano huo, kwani ni kinyume na maadili ya elimu ya juu nchini.

Kutokana na hilo, Tahliso katika taarifa yake, ilitamka bayana kuwa mkutano ulioitishwa Morogoro ni batili na hautambuliki kwa mujibu wa sheria namba 7 ya vyuo vikuu ya mwaka 2005, sheria ya mashirika yasiyokuwa ya Serikali namba 24 ya mwaka 2002 na Katiba ya Tahliso.

Na ilitoa onyo kwa viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu ambao walishiriki mkutano huo na kutaka wasirudie, “na vinara wa wanafunzi ambao walikuwa mstari wa mbele kuchochea masuala ya kisiasa bila kufuata utaratibu watawajibishwa ipasavyo”.

Ilipiga marufuku  wanafunzi au makundi ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kuendesha harakati za siasa kwa kutumia jina la chuo, vyuo au taasisi yoyote inayoshughulika na elimu ya juu nchini.

“Tahliso itawaandikia barua waadili wote wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na kuwapa hadidu za rejea kuhusu utaratibu wa kubaini vikao halali na batili ili kuratibu vema ruhusa kwa viongozi wa serikali za wanafunzi, ili kuhudhuria mikutano ambayo iko nje na taratibu za chuo husika na inayohusu masuala ya wanafunzi kitaifa au vinginevyo,” ilisema taarifa.

Ilikumbusha wanafunzi wa elimu ya juu nchini jukumu lao la kusoma na kujifunza taaluma zao kwa taratibu zilizoainishwa na chuo husika. “Hicho ndicho kilichowapeleka chuoni, kwa hiyo wafanye masomo kwanza, chama chao ni taaluma, kisha siasa wafanye baadaye”.



 

Tuesday, August 20, 2013

Viatu 590,000 vyagaiwa bure kwa wanafunzi

CHAMA  cha Msalaba Mwekundu Tanzania, kimegawa bure jozi 590,000 kwa wanafunzi wasio na uwezo kuvinunua katika mikoa saba nchini .

Ugawaji huo ulianza jana baada ya Rais wa Chama hicho, George Nangale kuzindua mradi wa viatu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Dar es Salaam.


Akizungumza  wakati wa uzinduzi huo, Nangale alisema viatu hivyo vyenye thamani  ya jumla ya tshs builioni 2.4 vimetolewa kwa chama hicho na kampuni ya Tom Shoes ya Marekani ili vigawiwe kwa wanafunzi wahitaji bila malipo yoyote.


“ Tumepokea kontena 50 za raba hizo na tayari zimekwisha tawanywa kwenye mikoa husika ikiwemo Dar es Salaam, Pwani na Kilimanjaro  tayari kuanza kupewa walengwa mara baada ya kuzindua mradi huu muda ( jana),” Nangale alisema.


Kwa maelezo yake, kampuni ya Tom Shoes imelenga kuwalinda wanafunzi hao na maradhi ya safura, minyoo na mengine yanayotokana na kukanyaga ardhini bila viatu.


“Katika Afrika Kenya, Malawi, Zambia zilipewa msaada kama huo na sasa  Tanzania imekumbukwa, watatuletea jozi nyingine milioni moja kabla ya mwisho wa mwezi ili tufikie mikoa yote bara, mikoa yote mitano ya Zanzibar iko kwenye hesabu ya jozi 590,000,” alisema.


Meneja mradi wa chama hicho alisema kampuni hiyo itaendelea kutoa msaada wa viatu kwa wanafunzi Tanzania iwapo masharti ya kuviuza na kutogawa kwa upendeleo yatazingatiwa . 


Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Afya wa chama hicho,  Bertha Mlay  msaada huo ni endelevu kwa miaka mitatu .
mwisho

Mama Pinda asikitikia matunzo duni ya wanafunzi wa kike


MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amesema ipo haja ya kuweka juhudi za makusudi za kuwezesha wasichana nchini kuondokana na aibu zinazowazuia kuhudhuria masomo yao kila siku.

Alisema  kukosekana kwa vifaa vya kujisitiri miongoni mwa wasichana waliofikia balehe, ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wakose masomo kati ya siku 30 hadi 70 kwa mwaka jambo ambalo linachangia kudorora kwa elimu miongoni mwao.


Alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua Mradi wa Hakuna Wasichoweza katika Shule ya Msingi Chilongola, iliyoko Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara.


Mradi huo unafadhiliwa na Taasisi ya T-MARC inayojihusisha na Masuala ya Afya na Maendeleo, umelenga kuwafikia wasichana 10,000 katika wilaya mbili za mkoa wa Mtwara, yaani Manispaa ya Mtwara Mikindani na Wilaya ya Mtwara Vijijini.


 “Wasichana wengi wanapopata siku zao, hushindwa kuhudhuria masomo yao kati ya siku tatu hadi saba kwa mwezi au siku kati ya siku 30 hadi 70 kwa mwaka. Hii husababishwa na wasichana hawa kukosa nyenzo za uhakika za kujisitiri wakiwa shuleni. Wengi wao huamua kubaki nyumbani hadi pale mzunguko wao utakapokwisha ili kuepuka kuaibika...,”  alisema.


Alisema usiri na ufahamu mdogo wa jamii kuhusu masuala ya hedhi na changamoto wanazozipata wasichana katika kipindi hiki pia ni tatizo kubwa.


“Wengi wetu katika jamii inayotuzunguka bado tunalichukulia suala la hedhi kuwa suala la aibu na la siri kubwa, kwa hiyo matatizo yanayotokana na hali hii ya kawaida hubaki bila kushugulikiwa, kwani kila mtu anaona aibu kusema wazi kuwa kuna tatizo,” aliongeza.


Vyuo vyatakiwa kupitia mitaalam yao



MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imevitaka vyuo vya elimu ya juu nchini, kuweka utaratibu wa kuipitia mitaala yao hasa katika eneo la mawasiliano iweze kwenda sanjari na kasi ya ukuaji wa teknolojia nchini.


Msemaji wa Mamlaka hiyo, Innocent Mungy,  alisema hayo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa progamu tatu za uzamili uliofanywa na Chuo cha Uhasibu cha Arusha (IAA) kwa kushirikiana na Chuo cha  Galgotias cha nchini India.


Mungy alisema taifa linapozidi kupiga hatua kimaendeleo katika nyanja za mawasiliano, ni vizuri vyuo vyote na hasa vya elimu ya juu vikaweka mkazo kuhakikisha  vinapitia vyema mitaala ya ufundishaji kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia yaliyopo.


“TCRA imekuwa ikitoa udhamini kwa wanafunzi mbalimbali katika fani za teknoham

a, hii  ni kwa lengo la kuwahamasisha zaidi ili waweze kutilia mkazo katika eneo hilo na hivyo kuongeza idadi ya wataalamu nchini,” alisema Mungy.

Akizungumzia uzinduzi wa programu hizo za uzamili katika masuala ya Kompyuta, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Profesa Johannes Monyo, alisema malengo ya chuo ni kuongeza idadi ya wataalamu katika fani hizo ili kuleta ushindani kimataifa.

Kasheshe la kugushi vyeti katika Dayosisi ya Pwani


WAKATI taifa linatafuta ‘dawa’ kukomesha udanganyifu katika mitihani na kughushi vyeti, kashfa imeibuka ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzannia (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani huku baadhi ya wachungaji wakituhumiwa kujipatia nafasi za utumishi pasipo kuwa na sifa za kitaaluma.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba zaidi ya wachungaji 20 ambao hivi sasa wanatumikia sharika mbali mbali nchini walidanganya juu ya ufaulu wao katika kidato cha Nne na cha Sita.

Kati ya watumishi hao ambao wamehitimu katika vyuo mbali mbali hapa nchini, inadaiwa kuwa watano wanahudumu katika sharika za hapa jijini Dar es Salaam.

Vyanzo vya habari vimebainisha kuwa wachungaji hao ambao walijiunga na vyuo vya Theolojia vya Mwika (Kilimanjaro), Kidugala (Iringa) vyote vikiwa chini ya Chuo Kikuu cha Tumaini baadhi yao wamepewa likizo ya lazima ya miezi miwili kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu.

Sakata hilo la kusaka uhalali wa vyeti vya wachungaji hao lilianza miezi sita iliyopita na kusababisha wawili kati ya watumishi hao kuondolewa kwenye utumishi.

Pia imebainika kuwa hivi karibuni msako uliendelea na kubaini kuwa wapo wachungaji wengine ambao ni watuhumiwa lakini bado wanaendelea na kazi ikidaiwa kuwa wanakingiwa kifua na baadhi ya viongozi wa juu wa kanisa hilo kwa misingi ya ukabila.

Imeelezwa kuwa baadhi ya watuhumiwa hao walitengeneza vyeti kuonyesha matokeo bandia tofauti na matokeo yao halisi wakati ambapo wengine hawakufika kidato cha Nne au cha Sita kabisa.

“Unakuta mtu anataka kwenda kusoma diploma ya Theolojia awe mchungaji wakati yeye amemaliza darasa la saba, anatengeneza cheti cha kidato cha nne ili apate sifa ya kwenda chuoni. Wengine wanatengeneza vyeti na kujiwekea alama mfano ‘B’ kuonyesha ufaulu mzuri kumbe sivyo. Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na vyuo walivyosoma vinapaswa kufuatilia uhalali wa diploma zao na kuchukua hatua stahiki,” chanzo kimebainisha.

Kufuatana na Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005 nafasi ya masomo inapatikana kwa wanafunzi waliokidhi vigezo vyote vya kujiunga na chuo baada ya udahili.

Pia ni marufuku kwa mwombaji yeyote kudanganya katika ufaulu wake katika ngazi zote hususan shule za sekondari.

Chanzo kingine cha habari hizo kimebainisha kuwa umekuwepo mvutano wa ndani kuhusu namna ya kulitatua tatizo hilo ambapo vyeti vya watuhumiwa vilibainika kuwa na kasoro ila wawili tu ndio wameondolewa kwenye utumishi na wengine kuendelea kukingiwa kifua na baadhi ya wakubwa.

Imebainika kuwa walioathirika na sakata hilo wanalalamika kuwa haki haijatendeka maana wapo wachungaji waliodanganya katika vyeti vyao lakini bado wanaendelea na kazi.

Mwumini mmoja Rabison Hojo (56) mkazi wa Kipawa, jijini Dar es Salaam ameshauri umakini katika udahili wa wanafunzi katika vyuo vyote hapa nchini kwa sababu wale wanaoghushi vyeti wanaziba nafasi za wale wanaostahili.

“Inasikitisha zaidi suala la kughushi linapojitokeza katika madhehebu ya kidini. Wachungaji ambao wanawatangazia watu msamaha wanategemewa kuwa waaminifu na wakweli katika mwenendo wa maisha yao. Tuhuma hizi ni nzito tena ni lazima zifuatiliwe kikamilifu,” amesema Hojo.

Alipohojiwa juu ya sakata hilo Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Tumaini ambaye pia ni Mkuu wa KKKT nchini, Askofu Dk Alex Malasusa amesema yeye hana habari kabisa na uwepo wa wachungaji walioghushi vyeti na angependa kulijua zaidi jambo hilo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya KKKT, Bw Ibrahim Kaduma amesema kamati yake ambayo imeundwa hivi karibuni na yeye kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wake ingependa kushughulikia kikamilifu malalamiko yoyote ya waumini ili kuepuka kulipaka matope kanisa hilo.

“Ningependa kujua zaidi undani wa jambo hili na kamati yangu itafuatilia kwa karibu sana kubaini ukweli wa tuhuma hizo,” amesema Kaduma.

Mwisho

Sunday, August 18, 2013

Elimu ya kujitambua katika kutumia fursa yatolewa Kigoma

  1. Msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya na mfanyabiashara,Ambwene Yesaya a.k.a AY akitoa ushuhuda wake na mifano mbalimbali  katika Semina ya Fursa,kuhusiana na fursa alizozipata na kuzifanyia kazi,na kumpelekea mafanikio aliyonayo mpaka sasa.



  1.  Mkali wa kughani mashairi hapa nchini,Mrisho Mpoto akifafanua jambo mbele ya wakazi wa mji wa kigoma,alipokuwa akiielezea mada mojawapo iliyohusiana na fursa mbalimbali.

  1. Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group,Ruge Mutahaba akimkaribisha mgeni rasmi wa semina hiyo,Mh Issa Machibya wakati wa uzinduzi wa semina ya Fursa,kulia kwake ni msanii mahiri wa kughani mashairi hapa nchini,Mrisho Mpoto ambae pia likuwa ni mmoja wa watoa mada kuhusiana na suala zima la Fursa.
  2.  
  3. Habari kamili
  4.  
  5. Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel imeunga mkono juhudi za kusaidia vijana kuchangamkia fursa, kampeni inayoendeshwa pia kupitia tamasha la Fiesta.

    Kampeni hizo ni za kuhamasisha vijana kuchangamkia fursa zilizopo nchini ambapo zitaendana na tamasha la Fiesta linaloendeshwa kwenye zaidi ya mikoa 13 kwa kushirikiana na Clouds Media Group.

    Katika kila mkoa kampeni hiyo itakuwa ikifanyika siku moja kabla ya siku ya tamasha la Fiesta.

    Kwa mkoa wa Kigoma alikuwepo msanii Mrisho Mpoto pamoja na Ambwene Yesaya, AY ambao kwa pamoja walikuwa kivutio katika kuhamasisha vijana kujituma na kuwa wabunifu katika kutumia fursa katika nyanja mbalimbali ikiwamo ya muziki.


    Mada zitakazojadiliwa kwenye semina hizo ni pamoja na ubunifu, ujasiriamali, Uongezaji thamani kwenye bidhaa au shughuli yoyote unayofanya pamoja na kujenga ushirikiano, uwekezaji pamoja na lugha.

    Akizungumzia semina hizo, Afsa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan, amesema kampuni yake imekuwa msitari wa mbele katika kuwawezesha vijana, na kwa semina hizi wanaamini vijana wengi watapata nafasi ya kuzitambua na kujifunza.

    ‘Tanzania ina fursa nyingi sana kwa vijana, na sisi Zantel tunaamini nafasi hii itakuwa muhimu kwa vijana kujifunza na kutambua fursa zilizopo kutoka kwa wataalamu mbalimbali’ alisema Khan.

    Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, alisema nchi ya Tanzania ina fursa nyingi lakini tatizo limekuwa ni namna ya kuzitumia fursa hizo.

    ‘Tumeandaa semina hizi kwa kutambua tatizo kubwa lilipo kwenye jamii yetu, umaskini na ukosefu wa ajira kwa vijana, jambo ambalo semina hizi zitaenda kutatua’ alisema Mutahaba.

    Mojawapo wa wazungumzaji kwenye semina hizo atakuwa Mrisho Mpoto, mwakilishi wa mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF), Ruge Mutahaba pamoja na wageni waalikwa mbalimbali.

    Kwa mwaka huu semina hizo zimeanzia mkoa wa Kigoma, katika Ukumbi wa Kibo Hall Park, na mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya.