Na Mwandishi wa Elimu Bora
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka huu kinaanza kutoa Shahada ya Kwanza ya Sayansi katika Petroli, Jiolojia na Uhandisi wa Mafuta.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kampuni ya General Electron (GE) na Chuo hicho kusaini makubaliano ya ushirikiano kuongeza wataalamu wa gesi na mafuta nchini.
Makubaliano hayo yalifikiwa mwishoni mwa wiki baada ya Makamu Mkuu wa UDSM Profesa Rwekaza Mukandala kusaini mkataba huo pamoja na Mwenyekiti wa Kampuni ya GE, John Rice ambaye alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya pande zote mbili kukubaliana kwamba Tanzania sasa ni mzalishaji wa mafuta na gesi Afrika Mashariki hivyo upo muhimu wa kuboresha mafunzo ya gesi na mafuta katika vyuo vya Tanzania.
Katika makubaliano hayo, wameazimia kuanzisha mtaala wenye ufanisi katika kufundisha masomo ya gesi na mafuta na kuwavutia pamoja na kuwapa ushiriki wakufunzi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wakufunzi kitaalamu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mukandala alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uhaba wa rasilimali watu wenye ujuzi unaohitajika katika kushiriki kikamilifu katika sekta ya gesi na mafuta.
“Makubaliano haya ni ishara ya mwanzo ya dhamira ya ushirikiano wa muda mrefu na wa faida kati ya taasisi zetu hizi mbili katika kutoa mafunzo ya wahandisi wenye ujuzi kwa ajili ya sekta ya mafuta na gesi nchini,” alisema.
Rice alisema kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi nchini kwa zaidi ya 10 ikisaidia miradi mbalimbali hasa ya kuzalisha umeme na sasa inaanzisha ofisi yake jijini Dar es Salaam ambapo tayari imeajiri Meneja wake Mkuu ili kuendesha shughuli zake.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment