Mafunzo yakiendelea kutoka KIU |
Mtaalamu akitoa somo |
Na Evance Ng'ingo
SUALA la dawa za kulevya linazidi kuchukua sura mpya kila kukicha ambapo serikali pamoja na wadau wengine kadhaa wamekuwa wakipambana katika kuhakikisha kuwa wanalitokomeza janga hilo.
Wadau mbalimbali wamekuwa wakiendeleza mapambano dhidi ya janga hilo kwa kutumia njia mbalimbali ambazo zinalenga kuondoa kabisa matumizi ya dawa za kulevya.
Licha ya juhudi hizo za wadau lakini bado kazi imekuwa ni ngumu katikakutimiza azma hiyo.
Chuo Kikuu cha Kampala, KIU, kimeliona tatizo hilo ambapo chenyewe kimeamua kuwasaidia wale ambao wameshaathirika na dawa hizo za kulevya.
Uamuzi huo unalenga kuwarejesha tena kwenye jamii wale ambao wameathiriwa na dawa za kulevya ambao jamii inaonekana kuwatenga.
Jamii imekuwa ikiwatenga waathirika wa dawa za kulevya na mwisho wa siku waathirika hao wamekuwa wakikosa msaada na kujikuta wakiendelea kujihusisha na dawa hizo.
Familia nyingi zimekuwa zikiona aibu kuwahifadhi waathirika wa dawa hizo na mwishoe wanaonekana kuwatenga hasa kwa kuwafukuza majumbani au kuwapeleka katika vituo vya kuhifadhia vijana waathirika wa dawa hizo.
Dhana hiyo ya familia kuona aibu katika kuwasaidia waathirika kwa dawa hizo ndio imepelekea chuo cha KIU kuanzidha kampeni ya End Shame, ikiwa na nia ya kumaliza aibu kuanzia ngazi za kifamilia hadi katika jamii.
Kumaliza huko aibu kunahusisha kwanza wanajamii wenyewe kuepuke suala la kuona aibu kushugulika na waathirika wa dawa hizo lakini pia hata kwa watumiaji wenyewe kuepuka aibu ya matumizi ya dawa hizo pia.
Aibu ambayo familia inaona kuwa imepata kutokana na matumizi ya dawa hizo za kulevya ndio imepelekea kuwapo kwa hali ya kuwasusa vijana wengi na kuwapeleka katika vituo vya kusaidia waathirika ambapo nako hali ni sio ya kuridhisha.
Wakiwa katika vituo hivyo vijana hao wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikikwamisha harakati za vijana hao kurejeshwa kwenye maisha yao ya kawaida.
Chuo Kikuu, KIU katika kuliona hilo kimeamua kuingia kiundani zaidi kukabiliana na changamoto hiyo ya ukosefu wa utaalamu katika kuwahudumia waathirika hao.
Kiu imeanza kwa kuwachuja wanafunzi wake sita wanaosoma kozi Ustawi wa Jamii chuoni hapo na kuwawezesha kuanza kufanya kazi za kujitolea katika vituo mbalimbali vya vya kusaidia watu walioathiriwa na dawa za kulevya jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi hao sita ni Cecilia Mihayo, Zenah Msuya, Florah Rafael, Clarence Lihundi, Rossie Kasanga, Clara Nahum.
Mratibu wa mpango huo chuoni hapo, Lauren Schmidt anasema kuwa mpango huo unalenga kutoa mchango wa chuo hicho katika kupambana na dawa za kulevya.
Anasema kuwa watakuwa na jukumu la kuwaelekeza vijana njia mbadala za kujitoa katika matumizi ya dawa hizo pamoja na kuwawaunganisha vijana hao na wenzao wengine ambao wameshaacha kutumia dawa hizo.
Anaongeza kuwa wanafunzi hao ni sehemu ya mkakati wa chuo hicho wa kujitoa katika kuwaihudumia jamii ya kitanzania chini ya mradi wake wa Center for Wellness and Social Innovation.
Anaongeza kuwa wanafunzi hao wameundishwa njia mbalimbali za kusaidia jamii kuanzia ushauri hadi masuala mengine muhimu katika jamii.
Anaongeza kuwa wameunganishwa na vituo mbalimbali vinavyosaidia watu walioathiriwa na dawa za kulevya na watafanya kazi kwa kushirikiana na watu wa vituoni humo.
Lakini pia anabainisha kuwa ni wakati mwafaka pia kwa wanafunzi hao nao kujifunza mengi zaidi kuhusiana na namna ya kukabiliana na dawa hizo pamoja na kujifunza kiundani zaidi tabia na sababu vijana kujihusisha na dawa hizo.
Anafafanua kuwa huo ni mradi endelevu ambapo utadumu kwa miaka mingi ijayo na unalenga zaidi kuwasaidia waathirika wanawake.
"Sisi chuo cha KIU tumeamua kuanzisha harakati za kukabiliana na mambo mengi ambayo ni mabaya katika jamii yani yale ambayo yanaathiri mustakabali wa maendeleo ya jamii ya kitanzania na hizi ni jitihada endelevu".
Anaongeza kuwa "mradi huu pia utatoa jicho la kipekee kwa wanawake walioathiriwa na dawa za kulevya ambao wengi wao wamekuwa hawapewi kipaumbele kabisa katika mapambano dhidi ya janga hili".
Clarence Lihundi ambae ni mmoja kati ya wanafunzi walio katika mradi huo anasema kuwa unatoa msingi mzuri wa kuisaidia jamii tangia wakiwa chuoni.
"Sisi kama wanafunzi tunakipongeza chuo hiki kwa kutuunganisha na vituo mbalimbali vinavyosaidia waathirika wa dawa za kulevya kwa kuwa tumepata wasaha wa kufanya kazi kwa vitendo zaidi" anasema Clarence.
Khamis Shuwira ambae ni meneja mradi wa kituo cha Chance to change Sober house kilichopo Mbezi anasema kuwa ujio wa wanafunzi hao katika kituo hicho ni sehemu mojawapo ya kuongeza nguvu katika kuwasaidia vijana kuachana na dawa hizo.
Anasema kuwa kwa kuwa wanafunzi hao ni vijana na wamefundishwa masuala mbalimbali katika kukabiliana na dawa hizo hivyo wataongeza nguvu katika ushauri wa kuwaepusha vijana kuendelea na matumizi hayo.
Lakini hata hivyo anaongeza kuwa waathirika wa dawa za kulevya pia wanatakiwa kuunganishwa kwa ukaribu zaidi na wataalamu wa afya, wanasheria pamoja na wahusika wengine.
Anasema kuwa katika vituo vingi hakuna wataalamu wa kutosha wa kutoa huduma za afya kwa waathirika hasa wengi wao hawapatikana katika muda mwafaka wanapokuwa wakitafutwa.
Anafafanua zaidi kuwa kuna wakati waathirika wanakabiliwa na magonjwa mengine kadhaa lakini wakihitaji msaada wa wataalamu wa afya kunakuwa na shida kuwapata.
"Madaktari wengi wanaomba fedha kwanza kila pale ambapo wakiwa wanaomba kuitwa kuja kusaidia vijana na sisi fedha sio kwamba tunazo ila tunavyanzo kidogo tu vya kifedha kuweza kugharamia" anasema kijana huyo.
Anaongeza kuwa "sasa kama ambavyo KIU imeamua kuwatoa wanafunzi wake kuja kusaidia harakati za kuwasaidia vijana basi ni sisi pia tunaona kuwa hata wadau wengine nao wafanye hivyo hivyo".
KIU imeanzisha mradi huo wa Center for Wellness and Social Innovation ambao umepania kuhusisha nguvu ya kitaaluma na kiutalaamu kutoka chuoni hapo katika kuisaidia jamii ya kitanzania.
=======================
0 comments:
Post a Comment