Chanzo gazeti la Habarileo
WANAFUNZI kutoka vyuo 10 vya elimu ya juu nchini, wamewasihi wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kurejea ndani ya Bunge Maalumu la Katiba kuendelea na majadiliano.
Waliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana jijini Dar es Salaam na kushutumu hatua yao ya kususia vikao vya Bunge hilo wakisema kitendo cha kueneza propaganda chafu kuhusu Katiba mpya nje ya ukumbi wa Bunge, hakikubaliki.
Kiongozi wa wanafunzi hao, Gulatone Masiga alisema umoja wa wanafunzi hao haukubaliani na kitendo hicho cha Ukawa cha kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma.
Alisema wanafunzi wanawaomba wabunge wanaounda umoja huo kuendelea na majadiliano yenye maridhiano ndani ya Bunge hatua itakayowafanya wathibitike kuwa walikuwa na dhamira ya dhati ya kuwapatia Watanzania Katiba mpya.
“Katiba mpya haitapatikana kwa Ukawa kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma. Tunawaomba warejee bungeni vinginevyo warejeshe posho walizochukua,'' alisema Masiga ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wanafunzi hao pia walipinga lugha za kuudhi na kashfa zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wa Ukawa kwa waasisi wa Taifa ambao waliweka msingi mzuri wa Taifa kwa kuwawezesha wananchi wakiwemo viongozi wa umoja huo, kupata elimu, kuwa na uhuru wa kujieleza na kupata huduma nyingine za jamii wanazoendelea kufaidika nazo mpaka sasa.
“Watanzania wanapaswa kufahamu kwamba Marekani, Uingereza na nchi nyingine zilizoendelea zina nguvu kubwa kutokana na umoja na mshikamano wao.
Kitendo cha baadhi yetu kufanya mchezo na Muungano wetu hakikubaliki hata kidogo,” alisema.
Kwa upande wake, mwanafunzi Dorcas Mwasunda kutoka Chuo cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE) alisema inawezekana Ukawa wakawa na hoja nzuri ya kutetea mfumo wa serikali tatu wanaoutaka lakini si vema kwao kutetea sababu hizo nje ya Bunge Maalumu la Katiba.
Alitaka wajumbe kukubaliana na kuheshimu pia maoni yanayotolewa na wajumbe walio wengi ndani ya Bunge hilo.
Akizungumzia ni kwanini hawakubaliani na mfumo wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya Katiba, Massoro Hussein Kivuga kutoka Chuo Kikuu cha St John’s, Tawi la Dar es Salaam alisema muundo huo bila ya kuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato utasababisha kuwa na Serikali dhaifu ya Muungano ambayo haitaweza kujiendesha.
Hatma ya Ukawa
Bunge Maalumu la Katiba linaendelea na vikao vyake mjini hapa ambavyo licha ya wajumbe kuendelea kujadili hoja kwenye taarifa za kamati, pia hatma ya wajumbe waliosusa Bunge hilo inatarajiwa kujulikana ndani ya wiki hii.
Hoja iliyoko mezani inayoendelea kuchangiwa na wajumbe ni kuhusu Kamati ya Bunge hilo namba moja hadi 12, juu ya Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba.
Wakati mjadala huo ukisubiriwa kuendelea, wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa ) waliosusa Bunge wiki iliyopita, wamekaririwa wakisisitiza kutorejea bungeni.
Hata hivyo wiki iliyopita, Mjumbe wa Bunge hilo Maalumu, Mwigulu Nchemba aliomba mwongozo akitaka Mwenyekiti wa Bunge kumwandikia barua Rais atengue uteuzi wa wajumbe waliounga mkono kauli ya mjumbe Profesa Ibrahim Lipumba ya kutoka nje ya Bunge wakati wa mjadala.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu alisema mwongozo huo utatolewa baadaye baada ya Kamati ya Bunge ya Uongozi kukutana kujadili jambo hilo, Alhamisi iliyopita.
Mwongozo huo haukutolewa baada ya kamati hiyo kukutana kwani Bunge liliahirishwa mchana siku hiyo kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka jambo ambalo linatarajiwa leo, mwongozo husika kutolewa bungeni.
Wajumbe wanaounda Ukawa, walitoka bungeni kwa kile walichodai wamechoshwa na ubaguzi na matusi dhidi ya CUF, Chadema na Wapemba ndani ya bunge hilo kunakofanywa na wajumbe wa upande wa walio wengi bungeni.
Mjadala
Ingawa haijulikani hatima ya Bunge hilo bila uwapo wa wajumbe hao wa Ukawa, wajumbe waliobaki wataendelea kuchangia hoja kwenye taarifa za Kamati ya Bunge hilo.
Sura ya kwanza ya rasimu hiyo ina sehemu mbili, moja inahusu jina, mipaka, alama, lugha na tunu za Taifa na sehemu ya pili inahusu mamlaka ya wananchi, utu na uhifadhi wa Katiba. Aidha, Sura ya sita inahusu Muundo wa Jamhuri ya Muungano.
Mgawanyiko
Mgawanyiko ulio ndani ya Bunge Maalumu la Katiba ni baina ya wanaounga mkono hoja ya kuwepo kwa muundo wa serikali mbili na wa serikali tatu. Kwa wanaounga mkono serikali mbili, wanasema ndiyo itakayodumisha na kuimarisha Muungano wa Tanzania na kwamba serikali tatu itavunja Muungano.
Kundi hilo linalounga mkono muundo huo linajiita Tanzania Kwanza na wajumbe wake ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), TLP , Chausta, Tadea, CCK, Jahazi Asilia, APPT-Maendeleo, UPDP, Wakulima AFP, UIND, ADC, SAU na baadhi ya wajumbe wa kundi la wajumbe 201 .
Kundi la pili ni lile linalounga mkono hoja ya serikali tatu ambalo ni wajumbe kutoka vyama vya Chadema, CUF, DP , NCCR-Mageuzi na baadhi ya vyama vingine vya siasa pamoja na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 walioteuliwa na Rais.
Kundi hilo la Ukawa ambalo hata hivyo limesisitiza halitarejea bungeni, hoja yao ni kuwa muundo wa serikali tatu ndiyo suluhu ya matatizo na kero za Muungano.
Madai ya Ukawa ni kwamba wajumbe wa Bunge wanaendekeza ubaguzi, matusi na rasimu inayojadiliwa siyo iliyowasilishwa na Tume.
Baada ya kususia Bunge hilo, siku iliyofuata, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta aliwataka warudi akisema kama lipo jambo, walipeleke kwenye Kamati ya Maridhiano lizungumzwe kwani kususia Bunge siyo sahihi.
Wajumbe hao wamesusia Bunge Maalumu la Katiba siku chache kabla ya kuahirishwa kwake Ijumaa wiki hii kupisha maandalizi ya Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza mwezi ujao. Bunge la Katiba litarejea tena Agosti mwaka huu.
Kamati ya Uongozi
Ingawa uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba haukupatikana jana kueleza hatma ya Bunge baada ya baadhi ya wajumbe kususa, taarifa zilizopatikana ni kwamba Kamati ya Uongozi imeshauri yatafutwe maridhiano.
0 comments:
Post a Comment