Na Mdau wa Elimu
MTIHANI wa kidato cha nne ulianza juzi nchini na takribani majuma mawili wanafunzi watakuwa kwenye pilika za hapa na pale za kufanya mtihani huo na kuhakikisha wanafaulu vema huku Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikiwa imetangaza viwango vipya vya ufaulu kuanzia mwaka huu. Ingawa marekebisho hayo ya viwango vya ufaulu yamefanyika, lakini bado kilio cha muda mrefu cha wadau wa elimu nchini ni cha mitaala ya kufundishia kubaki pale pale na bado ufumbuzi haujapatikana.
Upangaji huo wa Viwango vya Alama katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na cha sita pamoja na matumizi ya alama za tathmini endelevu ya mwanafunzi kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi huenda yakawa yamewapa faraja kubwa wanafunzi wetu, ambao hivi sasa wapo katika vyumba vya mtihani kutimiza wajibu wao. Faraja ambayo wanafunzi wameipata na hata katika pitapita zangu mtaani na katika mabasi ya jumuiya niliyopanda kwa siku hizi mbili ni kutokana na hayo marekebisho yaliyotangazwa na Wizara na hata wao wanasikika katika majadiliano yao kuwa sasa angalau ‘watapeta’ kutokana na marekebisho hayo
Pia walichekelea sana kuambiwa hakutakuwa tena na daraja ‘O’ ambalo lilikuwa likiwaaibisha sana wahitimu hao na mwaka jana baadhi yao walipoteza maisha kutokana na kupata daraja hilo na badala yake sasa kutakuwa na daraja la tano.
Lakini wakati wakishangilia hilo la kuwapo daraja la tano, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alikana Serikali kufuta daraja la sifuri akisema kulitokea mkanganyiko hivyo madaraja ya ufaulu kubaki I, II, III, IV na O, Hakuna Division V.
Lakini mimi nataka kusema kuwa kuwepo kwa daraja ziro au kutokuwepo hakutawasaidia wanafunzi wetu kwa lolote na badala yake wahakikishe wanafaulu vizuri na hilo daraja ambalo wanalichekelea lisipate mtu na wote waishie katika madaraja ya I-III au IV ikibidi.
Hata hivyo, hapo awali tulishuhudia alama za ufaulu za daraja la pili zikianzia 18-21 lakini sasa alama hizo zimeongezwa hadi 24, hii ni kuwa wale ambao walipata alama 22, 23 na 24 wakapata daraja la tatu sasa watapata la pili, hii ni kubebwa na katu hapa tunapunguza tu waliofeli lakini tusishangae kuona hata hizo wasizipate.
Pia alama 22-25 awali zilikuwa ni za daraja la tatu lakini sasa wanapanda hadi aliyekuwa akipata daraja la nne hapo awali kwa kupata 26-33 hivi sasa analetwa hadi daraja la tatu, mbeleko ya hali ya juu hii kutoka wizarani hakika wanafunzi wana haki ya kushangilia.
Wizara na wadau wake wa elimu wameona kuwa kuwapa watoto daraja la tano badala ya daraja sifuri kutapunguza machungu na huenda ikawa faraja kwao na kweli imekuwa maana wameshangilia na huenda mazombi wasichorwe mwaka huu, lakini alama 48-49 haikuwapo iliishia 35 tu.
Bila shaka wanafunzi mwaka huu hawatafanya vituko na vioja tulivyozoea kwa miaka ya hivi karibuni ya kuandika mistari ya mashairi, kuchora picha za Zombi hajavaa viatu na matusi na badala yake wataonesha ujuzi wao kwa kupata madaraja ambayo yamefanyiwa ukarabati isipokuwa wale wa daraja la kwanza tu.
Nimwaka wa Matokeo Makubwa Sasa ambayo ndio kaulimbiu ya Serikali baada ya ile ya Kilimo Kwanza kuanza kushika kutu kwa kasi ya ajabu bila mafanikio. Walimu nao hawana budi kuendelea kusisitiza na kusimamia vema mitihani ambayo sasa itakuwa myepesi kwa wanafunzi wao, laikini pia tujiepushe na udanganyifu na wizi wa mitihani hiyo kama tulivyozoea.
Wizi wa mitihani ya kidato cha nne nchini imekithiri na baadhi ya watu hawa wanaofaulu kwa kubebwa na mbeleko za hali ya juu wafikapo madarasa ya mbele hushika mkia darasani. Mwito kwa wanafunzi wote ni kufanya bidii katika kile ambacho wamejifunza kwa takribani miaka minne waliyokuwa shuleni, wengine wakisoma kwa raha huku wakipata huduma zote muhimu za shule na wengine wakisoma kwa jasho.