Na Mwandishi Wetu
WANAWAKE 29,
wajasiriamali katika nyanja tofauti tofauti wamehitimu mafunzo ya miezi 10 ya
ujasiriamali yaliyoandaliwa na Taasis ya Graca Machel.
Mafunzo hayo yamehusisha wanawake
wajasiriamali kuanzia ngazi ya chini ya kati na wajasiriamali wakubwa.
Akizungumzia kuhusiana
na mafunzo hayo, mratibu wa mafunzo hayo, Vida Mndolwa alisema, wajasiriamali
hao walikuwa wakisoma kila Alhamis ya mwisho wa mwezi na kuwa wapo wanafunzi
ambao waliishia njiani kutokana na sababu mbalimbali.
Alisema kuwa kwa
kipindi hicho chote wamefundishwa masuala mbalimbali yahusuyo biashara na kuwa
washiriki walikuwa na nafasi ya kujifunza zaidi kwa vitendo pia.
Kwa upande wake mgeni
rasmi katika ufungwaji wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wanawake nchini
(TWCC) Jacqueline Maleko, aliwataka wanawake hao kuwekeza zaidi kwenye mafunzo
kama hayo.
Pia aliwataka wanawake
kujenga utamaduni wa kufuatilia taarifa kuhusiana na masuala ya fursa za
kibiashara ili kuzitumia katika kupanua wigo wa shughuli zao.
Jacqueline alisema kuwa
wanawake wengi nchini wanashindwa kusonga mbele kibiashara kwa kuwa wanakosa
taarifa ambazo zingetumiwa kuwawezesha kusonga mbele kibiashara.
Alisema kuwa ili
kukabiliana na hali hiyo ni wakati mwafaka kwa wanawake kwenda kwenye vituo
mbalimbali vya kiuchumi au wizara na kuomba kupewa taarifa kuhusiana na miradi
ya kusaidia wanawake.
Alisema kuwa ipo miradi
19 ya kuwaendeleza wanawake na vijana kwa ujumla kiuchumi na kuwa kwa sasa
hakuna uwazi wa kutosha kuhusiana na miradi hiyo.
"Ni wakati sasa kwa
wanawake nchini kutafuta taarifa zitakazoinua biashara na hii ni hasa katika
kupata habari za fursa za kibiashara, waende Baraza la Taifa la Uwezeshaji
wananchi kiuchumi kuna mengi yanayohusiana na miradi ya maendeleo yanayoweza
kuwasaidia wwao kama wanawake" alisema Jacqueline.