Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHULE ya msingi Scholastica mkoani Kilimanjaro imetoa mwanafunzi bora wa kike katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 aliyekuwa miongoni mwa
wanafunzi 10 bora kitaifa waliopewa tuzo juzi mjini hapa na Makamu wa Rais, Dk
Mohamed Gharib
Bilal.
Mtoto huyo,Gladness Norbert (14) ambaye sasa anasoma Kidato cha Kwanza Shule ya Marian iliyoko Bagamoyo, Pwani, pamoja na wanafunzi wengine, wamepewa fedha taslimu na cheti.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Norbert Gwebe aliyemsindikiza mwanawe kuhudhuria hafla hiyo ya kukabidhi tuzo kwa shule, wanafunzi, halmashauri na mikoa iliyofanya vizuri,
alisema pamoja na kazi ya Mungu, wazazi wanao wajibu wa kulea watoto katika
misingi ya kupenda masomo.
Aidha alisema nidhamu ya shule inachangia kufanya mtoto afanye vizuri kwenye masomo.
Alisema pamoja na wazazi kuwa karibu na binti yao, mtoto huyo aliishi bweni ambako
pia alipata malezi bora yaliyomjengea nidhamu ya kupenda kusoma.
Akizungumzia mkakati wa wizara kutoa tuzo na zawadi kwa wanaofanya vizuri, mzazi huyo alipongeza hatua hiyo. “Hela hata kama ni ndogo, zawadi ni zawadi.
Imempa changamoto mwanangu ya kuendelea kufanya vizuri,” alisema.
Mtoto huyo, Gladness ambaye anaamini juhudi za walimu shuleni Scholastica pamoja na uwezo wa Mungu vimemfikisha hapa, aliahidi ataendelea kujitahidi kufanya vizuri
katika masomo yake ya sekondari.
Katikakilele cha maadhimisho ya wiki ya elimu kitaifa yaliyoambatana na utoaji tuzo,wanafunzi
10 bora waliofanya vizuri katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013
wakiwemo wasichana watano na wavulana, walipewa tuzo.
Pia wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri katika mtihani wa taifa elimu ya sekondari mwaka jana, wakiwemo wasichana watano na wavulana, walipewa tuzo.
Aidha shule 60 zilizoonesha maendeleo mazuri zilipata
fedha taslimu sh 3,000 kwa kila shule mahsusi kwa walimu waliochangia kuleta
maendeleo mazuri.
Makamu wa Rais, Dk Bilal aliasa wale wote waliopwa tuzo kuhakikisha wanadumu katika kufanya vizuri kwenye sekta ya elimu.